1 Samuel 28

Sauli Na Mchawi Wa Endori

1 aSiku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.”

2 bDaudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.”

Akishi akamjibu Daudi, “Vyema sana, mimi nitakufanya uwe mlinzi wangu daima.”

3 cWakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Israeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi.

4 dWafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa. 5 eSauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu. 6 fNdipo Sauli akauliza ushauri kwa Bwana, lakini Bwana hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu,
Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha.
wala kwa njia ya manabii.
7 hBasi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.”

Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.”

8 iHivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.”

9 jHuyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?”

10Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina la Bwana, akasema, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.”

11Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?”

Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.”

12 kYule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.”

13 lMfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?”

Yule mwanamke akasema, “Naona mungu unapanda kutoka ardhini.”

14 mSauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?”

Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.”

Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu kifudifudi, uso wake hadi ardhini.

15 nSamweli akamuuliza Sauli, “Kwa nini unanitaabisha kwa kunipandisha juu?”

Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena wala kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe la kufanya.”

16Samweli akamuuliza, “Kwa nini uniulize mimi, maadamu Bwana amekuacha na kuwa adui yako? 17 o Bwana ametenda lile alilotangulia kusema kupitia kwangu. Bwana ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa jirani zako, yaani Daudi. 18 pKwa sababu wewe hukumtii Bwana, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, Bwana amekutendea mambo haya leo. 19 qZaidi ya hayo, Bwana atawatia Israeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti, na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Bwana pia atalitia jeshi la Israeli mikononi mwa Wafilisti.”

20 rPapo hapo Sauli akaanguka chini, akajinyoosha, akiwa amejawa na hofu kwa ajili ya maneno ya Samweli. Nguvu zake zikamwishia kwa maana alikuwa hajala chochote mchana ule wote na usiku.

21 sYule mwanamke alipomwendea Sauli na kumwona amepatwa na hofu, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako mwanamke nimekutii. Nimeweka maisha yangu hatarini kwa kufanya kile ulichoniagiza nifanye. 22Sasa tafadhali isikilize sauti ya mtumishi wako, uniruhusu nikupatie chakula kidogo ule ili uwe na nguvu za kurejea ulikotoka.”

23 tAkakataa, akisema, “Mimi sitaki kula.”

Lakini watumishi wake wakaungana na yule mwanamke wakamsihi ale, naye akakubali. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.

24 uYule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona hapo nyumbani, akamchinja mara moja. Akachukua unga, akaukanda, akatengeneza mkate usio chachu. 25Ndipo akamwandalia meza Sauli pamoja na watu wake, nao wakala. Usiku ule ule wakainuka na kwenda zao.
Copyright information for SwhKC